Waraka wa Magavilla (Maoni)

Haya ni maoni ambayo nimekuwa nayo kwa kipindi cha muda mrefu na yana lengo mahususi la kuimarisha ufanisi wa kisiasa ama kupitia CCM, CHADEMA au vyama vingine lakini nimelenga hasa CHADEMA na CCM ili kufikisha maudhui yangu. 

Nimeandika waraka huu bila ya kupendelea chama chochote (ninaomba radhi kama utadhani waraka huu umeegemea upande mmoja) lakini ninakiri kuwa mawazo yangu huwa yana upendeleo wa pekee kwa Nyerere.

Siamini kwamba CHADEMA inatazamiwa na umma kwa kufuata vigezo vya mfumo wa “chama” kama ilivyo kwa chama cha CCM. Ni dhahiri kwamba CCM ni chama mahiri zaidi katika nyanja karibia zote za kimfumo labda isipokuwa kwa yale yaliyoifanya CHADEMA kuwa na ushawishi mkubwa katika miaka ya hivi karibuni. CHADEMA inawakilisha vuguvugu la mabadiliko ya umma kupinga mfumo tawala uliopo, ambao ni toleo la CCM , serikali ilizoziunda kwa zaidi ya nusu karne sasa na kusababisha tabaka la watu “wandani”.

Inaweza kusemekana kuwa mabadiliko haya yalichochewa zaidi na yaliyofanywa ama kutofanywa na CCM yenyewe kikiwa ni chama tawala kinachounda serikali. Hii haina maana kwamba CHADEMA haihusiki kabisa katika hili. Jitihada za awali za baadhi ya viongozi wa CHADEMA kama vile Dkt. Slaa, Mh Kabwe na wengineo katika bunge la mwaka 2005 zilizidi kuimarisha hali ya upinzani sio kwa maana ya “chama” tu bali zaidi kwa maana ya uwakilishi wa “sauti ya umma” ambayo watanzania wengi wamekuwa na shauku nayo kwa muda mrefu. Watanzania walichukulia CHADEMA kama chombo cha kupitishia mawazo na maoni yao ya upinzani dhidi ya mfumo huu wa utawala tofauti na CCM kilichokuwa kikitoa nafasi na kinachoendelea kutoa nafasi kwa hoja zenye kulinda maslahi ya chama tu.

Nyerere alithibitisha mwaka 1991/2 kwamba aina ya upinzani huu unaweza kutokea hata ndani ya chama (CCM) na bado ukaendelea kuwa na ufanisi mkubwa ila tangu mfumo wa vyama vingi uanze CCM imeuzima utaratibu huu.

Huu ni utambuzi ambao hauepukiki kwa vyama vyote katika kuendeleza mikakati yao kwenda mbele. Ni dhahiri kuna kitu, kama chama (CHADEMA) ambacho tangu kuanzishwa kwake kilikuwa kikihusishwa na kabila fulani tu kikapiga hatua hadi kufikia kukubalika katika karibia kila mji mkubwa wa Tanzania. CHADEMA haijajitofautisha kwa kuwa na itikadi ama mikakati ya pekee bali ni kwa umakini wao katika kubaini maovu yanayofanyika katika Taifa hili na ujasiri wao katika kuyapeleka hewana haya ndicho kilichofanya CHADEMA iwe sauti ya wanyonge na kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya jamii.

Ni muhimu kwa vyama vyetu vya siasa kukumbuka kwamba siasa sio “chama” tu na wala sio vinara wanaovipa umaarufu, bali ni watu (hususani watu wengi wa chini ambao ndiyo mhimili mkubwa wa usalama wa wachache walioko juu) na masuala ambayo yanawaathiri wao.

Simamia haya masuala na mengine yatajipa!


Leave Comments / Reviews