Mwalimu Nyerere - Roho Ya Taifa Utaifa, Demokrasia na Rais Tunayemuhitaji

Utaifa wetu ni imani yetu ya msingi inayotuunganisha kama watanzania. Imani hii inapandikizwa kama mbegu kwenye nyoyo hadi kuivaa nafsi na kuwa msingi wa mwongozo katika maisha yetu kama watanzania.

Dhana ya Utaifa inatokana na dhana ya nafsi. Asili yetu kama wanadamu inatulazimu kujumuika ili kuendelea na tunafanya hivi kwa kuzingatia mambo makuu mawili yanayotuunganisha: ubinadamu wetu (zao la Mungu) na uchumi wetu (zao la binadamu).

Hivi karibuni dunia imebadilika sana kiasi kwamba kiunganishi cha uchumi kimepewa kipaumbele zaidi na kusahau au kudogoza nafasi ya kiunganishi cha ubinadamu wetu.

Maungo ya kiuchumi yanategemea nguvu ya fedha wakati maungo ya ubinadamu wetu yanategemea nguvu ya roho - imani ya msingi inayokuongoza hata (na pengine zaidi) pale unapokuwa huna fedha.

Usione vinaelea ujue vimeundwa...

Janga kubwa linalokabili nchi zetu za Kiafrika ni kuiga mifumo ya kigeni bila kuelewa misingi yake. Na hakuna mfano mzuri wa hili kama dhana ya demokrasia.

Tumechorewa mipaka ya nchi zetu na badala ya kuwekeza kwenye Utaifa tukaingia kichwa kichwa na kuendesha nchi hizi kwa kutumia mifumo ya kigeni bila kubaini ukweli au ufanisi wa hii mifumo.

Tofauti na neno “Nchi”, ambalo linaelezea mipaka ya kiutawala, "Taifa" (Nation), ni kile kinachowapa watu sababu ya kujiona wamoja kiasi cha kuwa tayari kupigania na kulinda mipaka au nchi hiyo.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tofauti na viongozi wengine wa nchi za Kiafrika, wakati tunapata uhuru, alibaini mapema utofauti huo na athari zake na akajikita zaidi kwenye kujenga Utaifa kwa kuwasaidia Watanzania kujibu swali la “Sisi ni nani?” kwa kutumia Ujamaa na Azimio la Arusha kama msingi wa jibu la swali hili.

Pamoja na nchi kufuata sera za kijamaa pia sisi watanzania tuliishia kujitambua na kujitambulisha kama wanaujamaa.

Msingi huu imara wa Utaifa ndiyo unatoa nafasi kwa mtu yeyote kuwa na ushawishi kitaifa bila kuzingatia mifumo ya asili kama ukabila au udini. Tuna Marais ambao wametokea kwenye makabila madogo kabisa jambo ambalo ni ndoto kwa nchi karibia zote za Afrika kwa sababu ya kazi iliyotukuka alioifanya Mwalimu. Sisi mfumo wetu ni wa kitaifa na wala sio wa kidini wala wa kikabila.

Msingi na mwendelezo wa nchi yoyote ni uimara wa Utaifa wao.

Nchi yetu ilifanikiwa sana hata kiuchumi miaka kabla ya kupigana vita na Uganda kwa sababu tulikuwa wamoja kimwili na kiroho kama Taifa. Anguko la uchumi wetu halikutokana na sisi kujiita wanaujamaa au kuishi kiujamaa. Anguko la uchumi wetu miaka ya themanini lilitokana na kuiga na kuwekeza kwenye mifumo ya kigeni kiholela.

Baada ya kuipa kisogo  itikadi ya Ujamaa kwa maana ya mfumo wa kuendesha uchumi tukatupa jongoo na mti wake. Hapa ninamaanisha tuliachana na Ujamaa kama mfumo wa kiuchumi (jambo ambalo lilikuwa halikwepeki) na pia tukaachana na Ujamaa kama utambulisho wetu wa sisi ni nani kama watanzania (jambo ambalo halikuwa na ulazima).

Tukafika hatua mpaka tukalifuta somo la uraia kwenye elimu ya msingi tukijiaminisha kwamba elimu hiyo haina mchango wowote tena baada ya kuachana na mfumo wa Ujamaa.

Tukumbuke Utaifa ni sawa na imani nyingine, inapaswa kupandikizwa kwenye mioyo ya watanzania kama mbegu kuanzia elimu ya awali. Badala yake tukaukubali mfumo wa kidemokrasia bila kuelewa msingi wake.

Aliyewahi kuwa Rais wa Marekani Bwana Franklyn Rosevelt aliwahi kusema, ninamnukuu, “Ukweli ni muhimu sana kiasi cha kuhitaji kulindwa na jeshi la uongo”. Tujiulize, iweje demokrasia imestawi Marekani miaka yote ya uhuru wao (karne zaidi ya tatu sasa) ila karibia kote walikoieneza Afrika imechochea mpasuko zaidi badala ya kujenga umoja?

Demokrasia ni mfumo ulioundwa na mataifa ili kushirikisha wananchi walio wengi katika kuchagua na kuendesha serikali kama namna ya kuimarisha na sio kuuzorotesha umoja wa Kitaifa.

Kwa maana hii, siasa za ushindani kupitia mfumo wa demokrasia hazilengi kuligawa Taifa au kuhamasisha ubishani  usio na tija, la hasha! bali zinalenga kugawa Taifa kwa namna itakayoliungunanisha kama Taifa kwenye mambo ya msingi kama Tafsiri ya Utaifa wetu - “sisi ni nani?” na amani na umoja unaotokana na Utaifa wetu.

Kwa mfano, tunapenda kuwasifu wamarekani kwa siasa za ushindani ambazo haziathiri uzalendo wataifa lao.

Je, ni kwanini nchi ya Marekani yenyewe, pamoja na kuhamasisha siasa za utitiri wa vyama vingi huku kwetu kama kigezo cha kuwa na uhuru na demokrasia ya kweli, imetawaliwa na vyama vikuu viwili tu tangu wapate uhuru wao?

Kwa hiyo, inabidi utambue kwamba awali hivi vyama viwili vilikuwa ni chama kimoja; chama asisi - Republican Democratic Party na katika hatua za awali za Utaifa wao, walijikita zaidi kwenye kujengea heshima Utaifa wao na katunga katiba ambayo hadi leo ndiyo roho ya utaifa wao. Walipigana hadi vita ya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya wahaini waliotaka kubadilisha katiba hiyo.

Kwa maana hii, pamoja na kubadilishana madaraka kati ya vyama hivi viwili hawabadilishi imani yao ya msingi juu ya Utaifa wao ambayo imesimikwa kwenye Katiba yao.

Kwa Wamarekani Utaifa wao ni wazo lililoandikwa kwenye utangulizi wa Katiba yao - Azimio la Uhuru wao wakijitofautisha na Waingereza, ambao hawana Katiba ilioandikwa, huku Utaifa wao ukijikita kwenye utamaduni wao unaobebwa na ukoo wa Malkia (Mkuu wa Taifa).

Kwa kuzingatia umuhimu wa hizi alama kuu za Utaifa kama ukumbusho wa yale yanayowaunganisha kama Taifa, pia hizi alama zinapewa heshima ya pekee na kulindwa na siasa za kimazingira.

Je, sisi tunaheshimu nini?

Alama yetu inayotuunganisha na tunayoipanda kama mbegu kwenye nyoyo zetu kama roho ya Taifa ni ipi?

Katiba iliotumika kuasisi Taifa hili na ndiyo msingi wa Utaifa wetu tulitaka kuipeleka mrama kisiasa tena ikisindikizwa na matarumbeta. Yaani mgonjwa anaumwa kichwa unaona tiba ni kubadilisha moyo tena kwa kutumia fundi makanika badala ya daktari mbobezi?

Ukuu wetu wa nchi nao tumeshauweka rehani kila miaka kumi kwa kuuingiza kwenye siasa za ushindani? Je kuna ambaye amewahi kushuhudia Malkia akishambuliwa kisiasa tena ukizingatia utamaduni wa vyombo vya habari vya nchi hio kuwa ya kichochezi...

Heshima!

Sasa kama hizi alama mbili ambazo wenye kuasisi hii mifumo wanazijengea heshima kwa kutambua umuhimu wake kwenye kuunganisha watu kiuchumi na kiroho, sisi huku tunazigaragaza kwenye tope bila haya, ni kipi kinachotuunganisha kama alama ya Utaifa wetu Watanzania?

Kama mwili usivyojengwa kwa mkate pekee basi na Taifa haliwezi kujengwa kwa uchumi pekee; roho ya Taifa iko wapi?

Hata maandiko takatifu yanatusihi tuheshimu Baba na Mama kama miungu wetu hapa duniani. Baba na Mama ndiyo alama ya uanafamilia wetu na chanzo cha muungano wetu wa awali wa kiroho na kiuchumi. Kuwaheshima wazazi hata wawe na elimu gani au kiasi gani cha fedha, ndiyo msingi wa ujumuishi wetu tukianzia kwenye ngazi ya familia, ukoo, ukabila hadi kufikia Utaifa wetu.

Kwa bahati mbaya Nchi hii historia yake inafutika kabla haijaandikwa na vijana wengi wanatumika kisiasa kutokana na kutoijua historia ya nchi yetu. Kuna wanaotaka kutumia udhaifu huu wa uelewa na imani juu ya Utaifa wetu kama mtaji wa kisiasa hata kama itabidi kutugharimu Utaifa wetu.

Watu wa namna hii tuwaogope kama ukoma!

Maana wapo wanaopigania maendeleo na kuna wanaopigania madaraka na kipindi cha uchaguzi ni vigumu kuwajua. Ni sawa na kupima imani ya mtu akiwa ndani ya nyumba ya ibada tu bila kuzingatia mapito yake mtaani...

Roho yako ya asili inajidhihirisha pale ambapo umebanwa. Ni rahisi kujiamini kwamba wewe ni mtetezi wa Utaifa wetu mambo yakiwa shwari ila maji yakifika shingoni ndiyo tutajuana vizuri.

Tuchukulie mfano wa janga la Corona.

Corona imeathiri vibaya uchumi wa dunia na kujaza hofu zaidi ya matumaini kinyume na asili yetu wanadamu. Nchi nyingi zilifunga mipaka na kulazimisha watu kukaa ndani huku dawa za sili zikikejeliwa.

Msimamo wa Rais Dr. John Pombe Magufuli, pamoja na kutambua hatari iliyo kuwa wazi ya Corona na kuhamasisha hatua za msingi katika kukabiliana na janga hilo, pia ulitambua mamlaka ya Mungu na hali halisi ya Watanzania ambao wengi wao wanahitaji kutoka nje ili wapambane na hali zao kila kukicha na kuishi na akaelekeza maisha yaendelee na watu wafanye kazi kama kawaida.

Msimamo huu ulikumbwa na upinzani mkubwa ndani na nje ya nchi. Pamoja na upinzani huu mkali Rais John Pombe Magufuli, kwa uthubutu wake wa pekee, hakutetereka. Matunda yake tunayaona sasa. Tofauti na nchi nyingi duniani na hata jirani, Tanzania maisha yamerudi kuwa ya kawaida.

Tungefuata upepo na maneno ya hawa wapinzani tungekuwa na hali gani?

Ni suala la wakati tu.

Tanzania inahitaji Rais mahiri mwenye uthubutu wa kusimamia maslahi mapana ya Watanzania wa kawaida tujenge Tanzania tunayoihitaji ili kupata Tanzania tunayoitamani.

Maendeleo hayana upinzani. Ukiona mtu anapinga kila kitu hadi maendeleo yaliowazi ujue huyu anatafuta madaraka na sio maendeleo na kwa maana hiyo ni wa kumwogopa kuliko ukoma kama alivyotusihi Mwalimu Nyerere.

Tunavyoingia kwenye zoezi la kupiga kura, tunapaswa kuheshimu na kutanguliza Utaifa wetu. Kutengeneza uchumi ukiwa na Taifa imara ni rahisi kuliko kutengeza Taifa ukiwa na uchumi imara.


Leave Comments / Reviews