Miaka 7 ya utumwa – Ubinadamu Wetu Dhidi ya Uchumi Wetu na Shida ya Kuleta Maendeleo Afrika

Costantine Magavilla

"Roho ni injini ya maisha. Roho ni kichocheo unachokihitaji ili kuisukuma nafsi yako kuhimili msukumo wa kiuchumi huku ukiendelea kusimamia kile unachoamini kinahitajika ili kudumisha ubinadamu wetu. Roho ndio jambo kuu linalo tufanya tusichague kifo pamoja na ukweli kuwa ni chaguo linalo onekana rahisi."

“Nilifanikiwa kuvuka miaka 40 ya kuzaliwa mwezi uliopita” ni kauli inayo toa picha kamili juu ya mienendo ilioambatana na mapito umri huo. Maisha yangu yalivurugika kwa muda katika kipindi hiki ila nikavuka salama kiasi cha kuweza kuandika haya.

Sikuandika kitu chochote cha ukumbusho kwenye siku yangu ya kuzaliwa, mwaka huu, kwa mara ya kwanza tangu nianze safari hii miaka saba iliyopita, katika umri wa miaka 33 ambao pia ni umri wa Yesu kufariki (Hii ni ishara ya lengo langu kuu wakati huo).

Hivyo ‘barua hii’ sio tu kwamba ni chapisho langu la kwanza baada ya kutimiza umri huu wa miaka 40, lakini pia ni njia nzuri sana kwangu kuchangia tafakuri zako kuhusu mfungo unaofikia kikomo wa Kwaresima. Kufunga huku si tu muhimu kwa Ukristo, kama ishara, lakini pia ni muhimu kwa dini nyingi kwa kuwa unalenga kutoa mafunzo ya kujitoa (kujinyima), jambo ambalo ni muhimu zaidi katika mwendelezo wa ubinadamu wetu.

Nilipoandaliwa chakula cha jioni kwa ajili ya kusheherekea siku yangu ya kuzaliwa na familia yangu, wiki moja baada ya siku yenyewe, kwa sababu hawakuweza kukubali mwaka huu maalum upite kimyakimya; waliishia kwa kuniuliza kutimiza miaka arobaini kulimaanisha nini kwangu?

Nilishikwa na bumbuwazi kidogo kwa sababu sikutarajia swali kama hilo, nilitafakari na kujibu. Nikawaambia kwamba kutimiza miaka arobaini ninahisi ninajukumu la kuelezea kusudi langu kama Yesu alivyotufundisha miaka 2000 iliyopita wakati alipokufa akiwaacha wafuasi 12 tu; ili kusudi yako iwe na maana halisi inabidi idumu zaidi ya uhai wako na njia pekee ambayo itakayodumisha kusudi yako ni pale inapokuwa na maana kwa watu wengine na sio wewe tu. Kama alikuwa anathibitisha hili, kwa sasa ana wafuasi zaidi ya bilioni moja licha ya yeye mwenyewe kutokuwepo.

Katika kitabu changu kipya kiitwacho “Ubishi Komaa na Maisha” kilichoandikwa, kwa vipindi tofauti tofauti vya huu muda wa miaka saba, lakini bado hakijachapishwa; ninayagawa maisha katika sehemu nne. Lakini kiuhalisia maisha yanaweza kugawanywa zaidi na kwa ufanisi katika sehemu mbili tunapozingatia azma ya safari yako ya maisha na maana halisi ya kujitoa:
1. Miaka 40 ya awali. Nusu ya kwanza ya maisha yako ni kuhusu wewe, nguvu, uwezo wako na kadhalika na kuzitumia kuwekeza katika kuonyesha kusudi yako.
2. Miaka 40 ya kuhitimisha. Nusu ya pili ya maisha yako inachukulia kwamba mara tu utakapobaini na kuweka wazi kusudi yako, utaitumia kuwatumikia wengine zaidi ya kujitumikia mwenyewe.

Jambo moja ambalo nilijifunza mapema sana katika safari hii ndefu ya miaka saba ni kwamba maisha yangu yatafika mwisho ikiwa nitapenda au nisipende.

Hivyo kama kifo ni lazima, sasa kwa nini tunaishi?

Kusudi.

Kusudi ni sababu ya kuishi. Kusudi yetu itatuongoza katika njia mojawapo ya vielelezo viwili vinavyoshindana ambavyo vinafafanua maisha yetu - uwepo wetu kama binadamu (uhai) na /au mapambano ya kujiendeleza (kuishi). Kusudi yetu itaonekana kupitia muungano wowote kati ya haya miwili huku moja ikiitawala nyingine.

Kutokana na umauti wetu wa kibaiolojia usioepukika, tunajukumu, katika ubinadamu wetu, ili kuhakikisha kuwa kusudi yetu inaleta matokeo chanya kwa wengine, iwe kwa familia, marafiki au wafanyakazi; tunawajibu wa kudumisha kusudi yetu kwa namna ambayo italeta matokeo chanya kwa wengine.

Kwa hiyo tunapaswa kufanya nini?

Wekeza kwenye ‘roho’.

Roho ni injini ya maisha. Roho ni kichocheo unachokihitaji ili kuisukuma nafsi yako kuhimili msukumo wa kiuchumi huku ukiendelea kusimamia kile unachoamini kinahitajika ili kudumisha ubinadamu wetu. Roho ndio jambo kuu linalo tufanya tusichague kifo pamoja na ukweli kuwa ni chaguo linalo onekana rahisi. Ndiyo maana tunaimarisha nafsi kwa kunena mema na sio mabaya kwa sababu tunapoongea tunaongea na nafsi zetu.

Nusu mbili hizi za maisha yetu (kabla ya miaka arobaini na baada ya miaka arobaini) zinawakilisha pande mbili zinazokinzana katika maisha yetu (kuwepo na kuishi), zinazojionesha kupitia ubinadamu wetu na uchumi wetu, kwa mtiririko huo. Uwepo wetu kama binadamu (uhai) unategemea dhana ya ‘ubinadamu wetu’ na mapambano ya kuishi katika mazingira yetu (maisha) utegemea dhana ya ‘uchumi wetu’.

Cha kushangaza, uwepo wetu (uhai) ni kwa maslahi ya kijamii wakati mapambano ya kuishi (maisha) ni kwa maslahi ya mtu binafsi na matokeo yake, nusu yetu ya kwanza ya maisha inawezeshwa kwa nguvu ya msukumo wa kijamii (kujitoa kwa watu wengine kwa ajili yetu) utokanayo na ubinadamu wetu na hitaji la kuendeleza uwepo wetu kama jamii endelevu, wakati nusu yetu ya pili ya maisha inasukumwa zaidi na shauku binafsi (kujitoa kwetu kwa ajili ya watu wengine) inayosukumwa na mahitaji ya kiuchumi ili kuishi.

Hali hii ni ya kushangaza na pengine ni ya kuhuzunisha zaidi, kwa sababu wakati tunapoanza safari yetu inayotuwajibisha kimazingira kutenda zaidi kwa manufaa ya watu wengine na mwendelezo wa ubinaadamu wetu tukijua siku yetu ya umauti inakaribia, tunakuwa tumepewa uwezo wa kutosha kushikilia kilicho chetu na sio kutambua au kujali vya wengine. Hivyo tunapumbazwa na matukio ya wakati na kusahau maana ya hayo matukio isio fungamana na huo wakati.

Huu ndio mtego ambao umewakamata wengi Afrika kwa miongo kadhaa sasa. Wakati ambapo mataifa yetu yanatuhitaji zaidi, sisi, hasa wale ambao tuna uwezo wa kutosha wa kuchochea/kudhihirisha ajenda za kitaifa, tunapumbazwa na mapigano yetu wenyewe hata kwa gharama ya ubinadamu wetu wa pamoja.

Mimi, kwa hiari yangu, nilijiondoa kwenye mazingira ya ukuaji wa sekta ya mashirika binafsi kipindi hicho, pengine ilikuwa mapema sana, kama safari ya kiroho ili kulinda ufahamu wangu wa kusudi dhidi ya nguvu ambayo niliona ikifanikiwa taratibu kunielekeza katika kutafsiri kusudi yangu nje ya fikra zangu mwenyewe.

Niliwezaje kufanya hivi?

Niliwekeza kwenye dhamiri.

Niliwekeza katika dhamiri yangu kwa kujiunga na maisha ambayo yalinisukuma kushirikiana na wale ambao maisha yao yanaendana na malengo yangu, wale wasiokuwa na sauti ya kweli. Wale ambao simulizi yao mara nyingi tunaitumia ili kutekeleza malengo yetu wenyewe kwa gharama zao. Tunajifanya kama tunaongea kwa niaba yao wakati kiuhalisia tunaongelea nafsi zetu lakini kwa kutumia simulizi yao.
Tunahamaki kwa shida zao lakini kiuhalisia tunatumia hali na ujinga wao ili kurahisisha mapambano yetu ya kuishi. Nilifanya hivi kama njia ya kujikumbusha mwenyewe mahali ambapo yote haya yalipoanzia na labda muhimu zaidi kwa nini yote haya yalitokea kwa kuanzia. Tunafahamu ni muhimu kwa kiasi gani shida za watu kwenye simulizi yetu kwa ujumla. Hatupaswi kusahau hilo kamwe kwamba kabla ya Mataifa, kulikuwa na watu; hatimaye haiwezi kuwa kuhusu wewe bali itakuwa daima kuhusu sisi.

Kuwekeza katika dhamiri yako ni ulinzi muhimu zaidi dhidi ya matumizi mabaya ya roho (msukumo wa kuendeleza uwepo wetu kama binadamu) mbele ya mambano ya kuishi. Tunapokufa, ubinadamu wetu (uwezo wetu kuwepo kama wanadamu) huendelea kuishi kupitia misingi ambayo ilidhihirika wakati wa uhai wetu na uchumi wetu (uwezo wa kuishi kiuchumi) hufa mara moja na kulingana na uwekezaji tuliofanya katika ubinadamu wetu kupitia kwa wengine, hata ‘uchumi’ tunaouacha nyuma utakuwa hatarini kuangamia kwa nguvu hiyo hiyo.

Hii ni moja ya sababu kuu inayopelekea utajiri katika nchi hii kutokudumu baada ya walioitengeneza kutangulia mbele ya haki. Urithishaji wa utajiri kizazi kimoja kwenda kingine katika jamii yoyote ni zao la uwekezaji tunaoufanya katika ubinadamu unaotujumuisha dhidi ya uwekezaji tunaoufanya katika uchumi unaotujumuisha. Uwekezaji katika la kwanza lazima lizidi uwekezaji katika la pili endapo faida za hatua zilizopigwa za kibinadamu na kiuchumi zilizotokana na jamii zidumu baada ya uwepo wa kizazi kilichosababisha hatua hizo.

Hapa ndipo ambapo Afrika hufanya makosa kila mara. Nina amini mtanziko mkubwa wa Afrika ni kuyaona maendeleo kwa picha ya fedha, hali inayotokana na Afrika kuibuka wakati ambapo wengine ulimwenguni walikuwa wanavuna kutokana na faida zilizopatikana baada ya maelfu ya miaka ya kujenga ubinadamu wao zaidi kiasi cha kutoa fursa ya kutilia mkazo uchumi wao kuliko ubinadamu wao.

Hii ilikuja pamoja na mapinduzi ya viwanda na maendeleo katika teknolojia ya kompyuta ambayo hatimaye yalikuwa na athari za kufanya fedha ionekane kama ndiye kila kitu kwa mtazamo wa watu wa nje. Hivyo wakati Afrika (na nchi nyingi zinazoendelea) zilikuwa zikikua, kupitia Utandawazi (tofauti kabisa na Ubeberu ambao ulitangulia) fedha ilitangazwa kuwa mfalme na mtu yeyote aliyekuwa na mawazo tofauti (kama Mwalimu Nyerere wetu mwenyewe) hakuthaminiwa. Lakini tofauti na Asia, Afrika ilinunua hii picha kwa jumla na haraka na kukataa mfumo wetu wa kipekee wa ubinadamu (na hivyo dhana nzima ya ubinadamu) kwa kubadilishana na tamaa ya kujenga uchumi badala ya mataifa.

Mataifa, kama King Arthur, mwenye kuhusishwa zaidi na ustaarabu wa kisasa katika ulimwengu wa magharibi, alivyosema, yanajengwa kwa kujitoa.

Tanzania ya Mwalimu iliokoelewa kwa sababu hii tu. Alipinga mwenendo wa Afrika wa kutafuta mafanikio rahisi katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi na kufanikisha hili ilimaanisha kupunguza kasi ya mawimbi ya mabidiliko. Pamoja na ulimwengu wa magharibi kuwa kinyume kabisa na ujamaa/ukomunisti, walimtazama kwa mshangao na heshima bado, kwa kuwa Mwalimu aliidhihirisha na dhima yake ya kuthubutu. Mwalimu ameingia katika kumbukumbu za dunia kama Rais pekee aliyejenga Taifa kwa kuwaunganisha watu wa asili/kabila tofauti katika karne hii.

Muda nilioutumia nje ya kufanya kazi katika sekta ya mashirika binafsi kumehalalisha jina lililoniongoza katika kuandika makala hii ya “Miaka saba ya Utumwa” - mtumwa wa kutambua kama sio kulinda “kusudi” iliyowekwa na Mungu kwangu; au kama Oprah anavyosema - muongozo wangu ya kweli (true north).

Ninamshukuru Mungu wakati huu kwa kunipa nguvu ya kuvumilia miaka hii 7. Sasa baada ya kutimiza miaka 40 ninamwomba aniruhusu kutumia nguvu zangu za kuwasiliana, kuwa na uwezo wa kusambaza elimu iliyotokana na safari yangu kwa manufaa ya nchi hii na wananchi wake.

Kama nchi, tumependelewa kupita kipimo; lakini kama watu hatujielewi juu ya nini haswa kitakachotupeleka mbele zaidi.
Jambo la kwanza tunalohitaji kufanya ni kutibu ubinadamu wetu kama watu na kutambua bila shaka umuhimu wa kuendeleza mafanikio ya kazi yaliyofanywa na Mwalimu Nyerere na kizazi chake, katika kuyapelekea hayo mafanyikio.

Kwa leo, ninaishia hapa lakini mtarajia kusikia zaidi kutoka kwangu kwenda mbele zaidi.

Ninamaliza makala yangu ndefu kwa maneno niliyomwambia Diamond Platinumz, msanii mkubwa wa Tanzania, ambaye hivi karibuni aliipatia nchi yetu heshima ya kuzindua Songamusic ya Safaricom nchini Kenya; ushirikiano wa kipekee. Na ukweli ni kwamba ‘songa’ inaelezea mapambano yaliyoendelea kabla ya mafanikio yake inaelezea sana uzito uliowekwa kwenye mabega ya Diamond kuhamasisha vijana ku’songa’ kwa kutumia mapambano zaidi ya alama za mafanikio tu kama ilivyo sasa.

Nimesema na nitaendelea kusema kuwa mojawapo ya mafunzo makuu niliyojifunza katika maisha ni kwamba mapambano ni ustaarabu wetu wa asili na mafanikio ni kituo tu cha kuchochea msukumo wa roho kuelekea kwenye mapambano endelevu.
Tunapaswa kukumbuka daima kuwa kuendelea kuwepo kwetu na ubinadamu wetu kunahitaji tuwe na njaa lakini kamwe tusiingiliwe na tamaa; kuwa na tamaa kunamaanisha kuchukua hata wakati hautoi, wakati kuwa na njaa kunamaanisha kutoa hata bila kuchukua.

#kujitoa na #mapambano, #mafanikio, katika ubora wake, yanawezesha sio kusababisha.


Leave Comments / Reviews